
Duniani kote, watumiaji wa Wikimedia wenye haki za ziada hutumikia jumuiya za Wikimedia, wakifanya kazi kama watetezi wa mstari wa mbele wanaofanya kazi nyuma ya pazia ili kulinda uadilifu, ubora na usalama wa miradi. Kupitia matendo yao katika majukumu yao, wanaunda vyema utamaduni wa jamii na kuweka kanuni zinazoathiri watumiaji wapya na waliopo. Yeyote ambaye ametumia muda kwenye wiki amewaona wakifanya kazi– wakitinga kusuluhisha mijadala mikali, kurudisha nyuma mabadiliko mabaya, kutekeleza makubaliano ya jumuiya, kutekeleza sera za maadili, na kushughulikia majukumu mengine mengi.
Watumiaji wenye haki za ziada ni pamoja na wakabidhi, warasimu, watendaji (watumiajiwacheki na waangalizi), wasimamizi, na wengine wenye ufikiaji wa hali ya juu. Kwa ujumla wao huchaguliwa na kukabidhiwa na jumuiya kufanya kazi maalum, wakiwa na ufikiaji wa kiufundi kwa miradi ya Wikimedia. Kulingana na jukumu lao, watumiaji wanapewa ufikiaji wa ndani, maalum kwa wiki fulani, au haki za kimataifa.
Tofauti na majukwaa mengine mengi, watumiaji wa Wikimedia wenye haki za ziada ni, kama wachangiaji wote, watu wa kujitolea. Kazi yao mara nyingi huhitaji mchanganyiko wa ujuzi wa kiufundi, uongozi wa jamii, na kujitolea kudumisha na kuboresha maudhui kwenye miradi.
Pamoja na kuongezeka kwa taarifa za uongo na upotoshaji, uharibifu, na vitisho vya usalama, kazi ya watumiaji wenye haki za ziada haijawahi kuwa muhimu zaidi. Na bado, hitaji la michango yao linapoongezeka, idadi yao inapungua kwenye Wikipedia kubwa zaidi, kwa watu wachache wa kujitolea wanaoanza safari ya kuwa watumiaji wenye haki za ziada.
Ndiyo maana Shirika linawekeza katika kuleta watumiaji wengi wenye haki za ziada kuliko hapo awali kuunganishwa katika Wikimania mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.
Safarini kuelekea Nairobi
Kwa miaka mingi, jumuiya ya wahariri wa Wikimedia imeeleza haja ya usaidizi mkubwa zaidi kwa watumiaji wenye haki za ziada. Kadiri idadi yao inavyopungua na mzigo wa kazi unavyoongezeka, hitaji la usaidizi wa kiufundi na kijamii limedhihirika, sio tu kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi bali kuwaandikisha na kuwabakisha watu wapya wa kujitolea wanaoingia katika majukumu hayo.
Wikimania ya mwaka huu itafanyia majaribio tukio la mara moja la kabla ya mkutano mnamo tarehe 5 Agosti linalolenga watumiaji wenye haki za ziada. Tukio hili litakuwa mahali pa watumiaji kuunganishwa, kutafakari suluhu za matatizo, kujadili maeneo ya mkazo kwa kazi mpya ya ushirikiano, kujenga uwezo kwa kujifunza kutoka kwa kila mmoja wao, na kuunda mtandao wa usaidizi katika siku zijazo. Mada zitajumuisha usalama, faragha, zana za sera na ubadilishanaji wa uzoefu wa Wiki. Taarifa zaidi zitatolewa hivi karibuni kwenye Wikimania Wiki.

Kwa kutambua jinsi inavyoweza kuwa ghali kuhudhuria na kwa kuzingatia wajibu wetu unaoendelea wa Mpango wa Mwaka kwa wahariri wenye uzoefu na kufanya kazi ili kuunganisha harakati, Shirika la Wikimedia Foundation limepanua mpango wa ufadhili, likitoa jumla ya ufadhili 50 wa Wikimania kwa watumiaji wenye haki za ziada, ili waweze kuhudhuria siku hii pamoja na mkutano uliosalia. Tunaamini watumiaji wenye haki za ziada watakuwa na thamani ya kipekee ya kuongeza katika siku na mada zote za mikutano.
Mtumiaji:Icem4k, mkabidhi kwenye Wikipedia ya Chichewa, ni mmoja wa watumiaji 50 wenye haki za ziada ambaye amepata ufadhili wa kuhudhuria Wikimania mwaka huu. “Nilipogundua kwamba nilitunukiwa ufadhili huo, nilihisi kuheshimiwa na kushukuru sana,” alieleza. “Hii ni mara yangu ya kwanza kupokea ufadhili kutoka kwa Shirika la Wikimedia Foundation. Zaidi ya usaidizi wa kifedha, ufadhili huu unatumika kama uthibitisho wa kazi yangu, ukinitia moyo kuendelea kuchangia na kuleta matokeo chanya.”
Uwekezaji huu maalum pia utasaidia Ajenda ya Afrika ambayo inataka uhusiano zaidi kati ya jumuiya za Kiafrika na watumiaji wa kimataifa wenye haki za ziada. “Ninahisi msisimko mkubwa kujua kwamba nitakutana na watu wenye maslahi sawa kutoka duniani kote,” alisisitiza Mtumiaji:Fulani215, mkabidhi kwenye Wikipedia ya Fulfulde.
Ufadhili utagharamia usafiri, malazi, na usajili, na hivyo kuwapunguzia mzigo wa kifedha wale ambao pengine wasingeweza kuhudhuria. Uteuzi unatokana na michango kwenye miradi, ushiriki kwenye jumuiya, na uwezekano wa matokeo katika kazi zao ndani ya harakati.
Tukijiandaa kwa tukio la kabla ya mkutano, Mtumiaji:DaSupremo, mkabidhi kwenye Wikipedia ya Pijini ya Ghana, anatarajia kuona warsha zinazowasaidia waliohudhuria kwa mara ya kwanza kupitia Wikimania, kuelewa utawala wa Wikimedia, na kuungana na washauri. Pia wana hamu ya vipindi vya kiutendaji kwa wasanidi programu na waendeshaji roboti, mikutano ya kikanda na lugha, na mafunzo ya vitendo kuhusu jinsi ya kushughulikia mizozo na kukuza mazingira rafiki ya kuhariri.
Wikimania Nairobi, ijapokuwa ni Wikimania ya kwanza kutoa ufadhili maalum kwa watumiaji wenye haki za ziada, pia inatoa ufadhili zaidi kwa wote. Nambari za ufadhili zimekuwa zikiongezeka kila mwaka, kwa 117 huko Stockholm, 200 zikitolewa Singapore, 240 zikitolewa Katowice, na 300 zikitolewa mwaka huu, ikijumuisha ufadhili huu 50 unaotolewa kwa watumiaji wenye haki za ziada kama majaribio ya mara moja.
Kuimarisha jumuiya kupitia uhusiano
Wikimania Nairobi pia itaadhimisha uwasilishaji wa pili wa tuzo ya Mtendaji Bora wa Mwaka, iliyoanzishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2024, kutambua watumiaji wanaofanya kazi nyuma ya pazia ili kuhakikisha usalama, utendaji kazi mzuri na uendelevu wa miradi ya Wikimedia.
Mwaka jana, Vira Motorko, Mkabidhi wa Wikimedia ya Ukraini na msimamizi kwenye Wikipedia ya Ukraini , alitambuliwa kama Mtendaji Bora wa Mwaka kwa mchango wake bora katika kudumisha Wikipedia. Maneno yake yanathibitisha ukweli wa kimsingi kuhusu kazi hii: “Juhudi zinazowekezwa katika kujenga uhusiano mpya huleta matokeo muhimu zaidi kwa sababu mtu mmoja peke yake si shujaa.”
Uendelevu wa miradi ya Wikimedia hautegemei tu michango ya mtu binafsi bali juhudi za pamoja. Mwaka huu, Wikimania itatoa nafasi kwa watumiaji wenye haki za ziada kushughulikia mada muhimu pamoja, kuunga mkono juhudi zao za kuweka miradi hiyo kuwa salama, inayotegemewa na kufikiwa na vizazi vijavyo. Ikiwa wewe ni mtumiaji mwenye haki za ziada, tunatumai utajiunga nasi.

Can you help us translate this article?
In order for this article to reach as many people as possible we would like your help. Can you translate this article to get the message out?
Start translation